| Choo cha kuchimbwa kikitumiwa vizuri husaidia katika kupunguza ugonjwa wa kuhara pamoja na mkurupuko wa magonjwa mengine yanayotokana na uchafu wa mazingira. |
Na Monica okwany
Swala la usafi ni sehemu muhimu
katika maisha ya kila siku ya mwanadamu na inastahili kupewa kipaumbele ili
kuepukana na magonjwa yanayozuka katika mazingira ya makazi ya binadamu. Hali
hii ni kinyume katika wilaya ya Kuria Mashariki kwenye kaunti ya Migori ambapo
usafi umepuuzwa kwa miaka mingi.
Asubuhi na mapema Bi Matilda Gati
anaonekana akitoka katika nyumba yake ya vyumba viwili iliyoezekwa kwa nyasi
akielekea kando na kuchutama kwenye kichaka yenye urefu wa mita kwenda haja
ndogo .
Anatekeleza kitendo hicho akiwa na
hofu ya kuonekana na mtu kwa sababu hana choo kilichochimbwa nyumbani mwake.
Wakati huo huo mita mia moja kutoka
hapo, Bw. Peter Mosasi Mwita anadamka na kujitosa kwenye kichaka kilichoko
nyuma ya nyumba yake na kuenda haja kubwa. Anachukua muda kujisafisha hali
ambayo inachafua mazingira ya hewa safi kutokana na uchafu aliyouacha nyuma.
Pia kwake kunakosekana choo cha nyumbani cha kuwezesha familia yake kujisaidia
kwa njia ifaayo.
Mambo haya yanafanyika katika
vitongoji vya eneo hilo na kuathiri mazingira yanayosababisha uchafuzi wa mito
na makazi ya binadamu ambayo imesheheni uvundo unayotokana na kinyesi.
Uchafu unaotokana na mabaki ya
vyakula na vinyesi imefanya wakaazi katika eneo hili kuhatarisha maisha ya
wengi, kile kinachojulikana na wataalamu wa maswala ya afya kama ‘kusababisha
vifo vya lazima kutokana na mkurupuko wa magonjwa yanayoweza kuzuilika.’
Wakaazi wa eneo hili wamekosa njia
mwafaka ya kutupa taka kwa kisingizio cha kukosa vyoo vilivyochimbwa nyumbani.
Ni kwa sababu hii wizara ya afya ya
umma na usafi ilijitolea kutoa mafunzo ya kipindi kifupi ili kuimarisha hali ya
usafi katika vijiji kwa lengo la kupambana na udororaji wa usafi katika maeneo
haya.
Hii kulingana na maafisa wa wizara
hiyo itatekelezwa kwa ushirikiano na shirika lisilo la kiserikali la APHIA-PLUS
mpanngo unaonuia kupata asilimia mia moja ya utumizi wa vyoo kwenye eneo hilo
kufikia mwisho wa mwezi wa Agosti mwaka huu.
Afisa wa mradi huo Bw. James Otieno amesema kwamba uzinduzi wa mradi huo
almaarufu kama “Community Led Total Sanitation (CLTS), itahakikisha kuwa kila
nyumba katika eneo hilo inapata choo cha kutumia.
Kwa hivi sasa ukadiriaji wa vyoo
katika wilaya hiyo ni asilimia 39.8 ambayo kulingana na wataalamu wa afya ni
cha chini mno na kuweka wakaazi wa eneo hilo kwenye hatari ya kuambukizwa
magonjwa ya kipindupindu na homa ya tumbo.
Bw Otieno katika mahojiano na KNA katika eneo hilo alisema utafiti uliofanyika hivi karibuni umeonyesha jinsi wakaazi wa eneo hilo walivyo kwenye hatari ya kuambukizwa magonjwa ya unywaji wa maji chafu inayotokana na uchafuzi wa hali ya juu ya mazingira kwa ujumla na vyanzo vya maji.
“Hali hii ndiyo imesababisha serikali kushirikiana na mashirika jirani kuhakikisha kwamba kila jamii imepata njia mwafaka ya kuhifadhi uchafu kwa kuwapa vifaa vifaavyo kwa matumizi hayo kwa sehemu zifaazo,” alidokeza haya wakati akizungumza na wanahabari katika afisi yake mjini Kegonga.
Afisa huyo alisema kwamba matumizi
ya vyoo ni muhimu sana katika maisha ya wengi na mradi huo utaimarisha namna ya
kuhifadhi uchafu unaotokana na shughuli za kibinadamu.Bw Otieno katika mahojiano na KNA katika eneo hilo alisema utafiti uliofanyika hivi karibuni umeonyesha jinsi wakaazi wa eneo hilo walivyo kwenye hatari ya kuambukizwa magonjwa ya unywaji wa maji chafu inayotokana na uchafuzi wa hali ya juu ya mazingira kwa ujumla na vyanzo vya maji.
“Hali hii ndiyo imesababisha serikali kushirikiana na mashirika jirani kuhakikisha kwamba kila jamii imepata njia mwafaka ya kuhifadhi uchafu kwa kuwapa vifaa vifaavyo kwa matumizi hayo kwa sehemu zifaazo,” alidokeza haya wakati akizungumza na wanahabari katika afisi yake mjini Kegonga.
Mradi huo ambao kwa wakati huu umeanzishwa katika tarafa ya Kegonga umewapa zaidi ya nyumba 100 ambazo hazikuwa na vyoo vifaa muhimu katika miezi mitatu iliyopita.
“Tunanuia kufikia sehemu kama
taarafa za Kwiho na Ntimaru kufikia mwanzo wa mwaka ujao,” Bw. Otieno amesema
huku akitoa changamoto kwa wakaazi wa maeneo hayo kuwa na mazoea ya kutumia
vyoo na kushiriki kikamilifu katika utunzaji wa mazingira yao.
Japo mradi huo utakumbwa na
changamoto ya kuwashawishi baadhi ya wakaazi wanaoshikilia dhana potovu kwamba
kutumia vyoo husababisha vifo kama inavyoaminika na wengi.
Kwa wakaazi wengine kutumia choo
kimoja katika familia moja ni kinyume na kaida za jamii na adhabu ya kwenda
kinyume ni kifo.
“Maishani mwangu sijawahi kutumia
choo kwa sababu ni hatia ambayo inaadhibiwa kwa kifo,” Bw Wantai Chacha alidai
wakati akihojiwa.
“Unawezaje kutumia choo kimoja na
watoto, wana na wakaza mwana wako na bado uwe na matumaini ya kuishi?”
alishangaa Bw Chacha.
Kando na mila inayohusishwa na
matumizi ya vyoo, kuna wale ambao wamekosa kuchimba vyoo majumbani mwao
kutokana na hali ngumu ya kimaisha.
‘Ni ujinga kuharibu pesa katika
kujenga choo wakati huna chumba cha kuishi,’ alisema Bw Gichoro katika
mahojiano.
Baadhi ya wakaazi wa eneo hili ni
wachochole kupindukia na wanaishi katika vyumba vikuu kuu vilivyoezekwa kwa
nyasi na hivyo hawaoni haja ya kuwa na choo wakati kuna majani ambayo
yamezingira majumba yao, alisema Bw Otieno.
“Lakini tumegundua kwamba wengi wa
wakaazi wa eneo hilo ni wazembe na pia wamekosa kuhamasishwa kuhusiana na
umuhimu wa kuwa na vyoo katika majumbani mwao,” aliongezea Bw Otieno.
