Tuesday, 9 October 2012

Mazingira safi kupunguza magonjwa

Choo cha kuchimbwa kikitumiwa vizuri husaidia katika kupunguza ugonjwa wa kuhara pamoja na mkurupuko wa magonjwa mengine yanayotokana na uchafu wa mazingira.

Na Monica okwany

Swala la usafi ni sehemu muhimu katika maisha ya kila siku ya mwanadamu na inastahili kupewa kipaumbele ili kuepukana na magonjwa yanayozuka katika mazingira ya makazi ya binadamu. Hali hii ni kinyume katika wilaya ya Kuria Mashariki kwenye kaunti ya Migori ambapo usafi umepuuzwa kwa miaka mingi.

Asubuhi na mapema Bi Matilda Gati anaonekana akitoka katika nyumba yake ya vyumba viwili iliyoezekwa kwa nyasi akielekea kando na kuchutama kwenye kichaka yenye urefu wa mita kwenda haja ndogo .

Anatekeleza kitendo hicho akiwa na hofu ya kuonekana na mtu kwa sababu hana choo kilichochimbwa nyumbani mwake.

Wakati huo huo mita mia moja kutoka hapo, Bw. Peter Mosasi Mwita anadamka na kujitosa kwenye kichaka kilichoko nyuma ya nyumba yake na kuenda haja kubwa. Anachukua muda kujisafisha hali ambayo inachafua mazingira ya hewa safi kutokana na uchafu aliyouacha nyuma. Pia kwake kunakosekana choo cha nyumbani cha kuwezesha familia yake kujisaidia kwa njia ifaayo.

Mambo haya yanafanyika katika vitongoji vya eneo hilo na kuathiri mazingira yanayosababisha uchafuzi wa mito na makazi ya binadamu ambayo imesheheni uvundo unayotokana na kinyesi.

Uchafu unaotokana na mabaki ya vyakula na vinyesi imefanya wakaazi katika eneo hili kuhatarisha maisha ya wengi, kile kinachojulikana na wataalamu wa maswala ya afya kama ‘kusababisha vifo vya lazima kutokana na mkurupuko wa magonjwa yanayoweza kuzuilika.’

Wakaazi wa eneo hili wamekosa njia mwafaka ya kutupa taka kwa kisingizio cha kukosa vyoo vilivyochimbwa nyumbani.

Ni kwa sababu hii wizara ya afya ya umma na usafi ilijitolea kutoa mafunzo ya kipindi kifupi ili kuimarisha hali ya usafi katika vijiji kwa lengo la kupambana na udororaji wa usafi katika maeneo haya.

Hii kulingana na maafisa wa wizara hiyo itatekelezwa kwa ushirikiano na shirika lisilo la kiserikali la APHIA-PLUS mpanngo unaonuia kupata asilimia mia moja ya utumizi wa vyoo kwenye eneo hilo kufikia mwisho wa mwezi wa Agosti mwaka huu.
Afisa wa mradi huo Bw. James Otieno amesema kwamba uzinduzi wa mradi huo almaarufu kama “Community Led Total Sanitation (CLTS), itahakikisha kuwa kila nyumba katika eneo hilo inapata choo cha kutumia.

Kwa hivi sasa ukadiriaji wa vyoo katika wilaya hiyo ni asilimia 39.8 ambayo kulingana na wataalamu wa afya ni cha chini mno na kuweka wakaazi wa eneo hilo kwenye hatari ya kuambukizwa magonjwa ya kipindupindu na homa ya tumbo.

Bw Otieno katika mahojiano na KNA katika eneo hilo alisema utafiti uliofanyika hivi karibuni umeonyesha jinsi wakaazi wa eneo hilo walivyo kwenye hatari ya kuambukizwa magonjwa ya unywaji wa maji chafu inayotokana na uchafuzi wa hali ya juu ya mazingira kwa ujumla na vyanzo vya maji.

“Hali hii ndiyo imesababisha serikali kushirikiana na mashirika jirani kuhakikisha kwamba kila jamii imepata njia mwafaka ya kuhifadhi uchafu kwa kuwapa vifaa vifaavyo kwa matumizi hayo kwa sehemu zifaazo,” alidokeza haya wakati akizungumza na wanahabari katika afisi yake mjini Kegonga.
Afisa huyo alisema kwamba matumizi ya vyoo ni muhimu sana katika maisha ya wengi na mradi huo utaimarisha namna ya kuhifadhi uchafu unaotokana na shughuli za kibinadamu.
Mradi huo ambao kwa wakati huu umeanzishwa katika tarafa ya Kegonga umewapa zaidi ya nyumba 100 ambazo hazikuwa na vyoo vifaa muhimu katika miezi mitatu iliyopita.

“Tunanuia kufikia sehemu kama taarafa za Kwiho na Ntimaru kufikia mwanzo wa mwaka ujao,” Bw. Otieno amesema huku akitoa changamoto kwa wakaazi wa maeneo hayo kuwa na mazoea ya kutumia vyoo na kushiriki kikamilifu katika utunzaji wa mazingira yao.

Japo mradi huo utakumbwa na changamoto ya kuwashawishi baadhi ya wakaazi wanaoshikilia dhana potovu kwamba kutumia vyoo husababisha vifo kama inavyoaminika na wengi.

Kwa wakaazi wengine kutumia choo kimoja katika familia moja ni kinyume na kaida za jamii na adhabu ya kwenda kinyume ni kifo.

“Maishani mwangu sijawahi kutumia choo kwa sababu ni hatia ambayo inaadhibiwa kwa kifo,” Bw Wantai Chacha alidai wakati akihojiwa.

“Unawezaje kutumia choo kimoja na watoto, wana na wakaza mwana wako na bado uwe na matumaini ya kuishi?” alishangaa Bw Chacha.
Kando na mila inayohusishwa na matumizi ya vyoo, kuna wale ambao wamekosa kuchimba vyoo majumbani mwao kutokana na hali ngumu ya kimaisha.

‘Ni ujinga kuharibu pesa katika kujenga choo wakati huna chumba cha kuishi,’ alisema Bw Gichoro katika mahojiano.

Baadhi ya wakaazi wa eneo hili ni wachochole kupindukia na wanaishi katika vyumba vikuu kuu vilivyoezekwa kwa nyasi na hivyo hawaoni haja ya kuwa na choo wakati kuna majani ambayo yamezingira majumba yao, alisema Bw Otieno.

“Lakini tumegundua kwamba wengi wa wakaazi wa eneo hilo ni wazembe na pia wamekosa kuhamasishwa kuhusiana na umuhimu wa kuwa na vyoo katika majumbani mwao,” aliongezea Bw Otieno.

No comments:

Post a Comment